Rais Suluhu aangazia umoja wa Wakenya na Watanzania katika hotuba yake kwa Bunge
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa Wakenya na Watanzania kuungana na kutangamana ili kuhamasisha uhusiano wao wa kibiashara na udugu.
Akihutubia Wabunge takribani mia moja na hamsini kutoka kwa Mabunge yote mawili katika Kikao cha Pamoja cha Bunge, Rais Suluhu aliangazia sana faida za muungano wa Wakenya na Watanzania katika ngazi mbalimbali.
Rais Suluhu alikemea mitazamo ya awali ya wananchi wa nchi zote mbili haswa wanasiasa, ambayo imechangia sana katika kuleta migawanyiko kati ya Kenya na Tanzania.
Akitoa shukrani zake kwa Wabunge kwa kumpa fursa ya kuwahutubia, Rais Suluhu alieleza furaha yake kwa maspika wa Bunge kwa kutunukiwa nafasi ya kuhutubia Kikao cha Pamoja cha Bunge. Hali kadhalika, alimmiminia sifa mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta kwa mwaliko wake wa kipekee. Alieleza kwamba alifarajika sana kwa kupata nafasi hiyo mwanzoni mwa uongozi wake huku akisema kuwa kumbukumbu hiyo na taadhima aliyopewa haitafutika kwenye maisha yake.
Akiangazia uhusiano baina ya nchi za Kenya na Tanzania, Rais Suluhu alibainisha kwamba nchi zote mbili zinakubaliana katika mambo mengi kuliko yale machache sana ambayo wanatofautiana. Aliendelea kusema kwamba hata hivyo, hayo machache hayajakuwa ya msingi bali ni mitazamo tu.
Akirejerea mazungumzo yake na mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta, Rais Suluhu ambaye ni wa pili kuhutubia Kikao cha Pamoja cha Bunge la Kenya aliwajulisha wabunge kuhusu makubaliano yao katika mazungumzo yao ya faragha hapo jana kwenye ikulu ikiwemo mwito wa kukutana mara kwa mara ili kuimarisha uhusiano wa nchi hizi mbili.
"Ili kuondoa mitazamo hasi kati yetu, tumekubaliana kujenga na kuendeleza utamaduni wa kukutana mara kwa mara, katika ngazi mbali mbali. Ndugu wa Jirani wanaotembeleana hujenga ukaribu kuliko wale wasiotembeleana. Umbali hutengeneza mashaka; ukaribu huyaondosha", Rais Suluhu alisema.
Rais Suluhu ambaye alifika Bunge takribani saa 8:45 mchana na kulakiwa na Maspika wa Bunge ya Taifa na Seneti pamoja na viongozi wengine bungeni. Pia, Rais Suluhu alielezea furaha yake kwa mwaliko wa kuhutubia Bunge. Alisema kwamba ilipendeza sana kuwa alipata nafasi ya kipekee sio tu kutembelea nchi ya Kenya kwenye Ziara yake Rasmi ya Kwanza, bali pia kwa taadhima ya kuingia kwenye kumbukumbu kama Rais wa Pili katika historia kuhutubia Kikao cha Pamoja cha Bunge la Kenya.
Akitaja taadhima aliyopewa tangu alipowasili nchini Kenya kuwa ya hali ya juu, alichukua nafasi kwenye jukwaa kuwahimiza wabunge kuwa kipao mbele katika kuhimiza umoja na uhusiano mwema wa nchi hizi mbili. Alitoa mwito pia kwa Wabunge kujizatiti kuwatumikia wanaowakilisha na pia kuhimiza serikali za nchi zote mbili kutilia maanani sera ambazo zitaboresha maisha yao na uhusiano wao.
Mheshimiwa Rais Suluhu alitaja kwamba uhusiano wa Tanzania na Kenya uliofungwa kwa mafundo matatu ni wa kipekee sana. Alielezea kwamba mafundo haya ni udugu wa damu kati ya wananchi wa nchi hizi mbili, wa kihistoria na pia wa jiografia. Alikadiria kwamba kutokana na ukweli huu, ushirikiano wa Wakenya na Watanzania si wa hiari bali ni wa lazima kutokana na kanuni za uasili wa udugu ambao Mungu ameuumba.
Pengine kwa jambo ambalo wabunge walingoja kulisikia sana, Rais Suluhu aliahidi kwamba katika awamu yake ya uongozi, atahakikisha kwamba Kenya inabaki kuwa ndugu, jirani, mshirika na mkakati wa mbia. Pia aliwahakikishia Wabunge kuwa Tanzania itaendelea kuwa jirani, mbia na rafiki mwaminifu na wa kutumainiwa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Hotuba ya Rais Suluhu iliyochukua muda wa saa moja ilihanikiza furaha na mbwembwe kwa Wabunge ambao walimshangilia kwa kupigisha miguu kama ilivyo kawaida ya kushabikia mambo bungeni.
Labda kudhibitisha kuwa ziara yake Bungeni ilikuwa ya baraka kama alivyotaja, baada tu ya kumaliza hotuba yake, mvua kubwa ilimwagika na kusitisha kidogo shughuli za kumuaga rasmi kwa muda. Baada ya kukaa faraghani kwa muda, Maspika wa Bunge walimuaga takribani saa 10.20. alasiri.